Staa wa Kiwanda cha Filamu Bongo, Irene Uwoya ambaye hivi karibuni alijifungua mtoto wa kiume, ametoa somo kwa wasanii wenye majina makubwa nchini, kuacha tabia ya kutoa mimba kwa sababu kitendo hicho siyo kizuri, Ijumaa linashuka na mkoba wenye ishu nzima.
Akizungumza na gazeti hili katikati ya wiki hii nyumbani kwao Mbezi, jijini Dar es Salaam alipotembelewa na mwandishi wetu, Irene alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu aliyewajalia kupata mtoto huyo ambaye amewatengezea heshima kubwa.
“Kusema ukweli mimi na mume wangu tunamshukuru sana Mungu, ametupa mtoto huyu, naamini amesababisha kuongezeka kwa heshima katika jamii,” alisema Uwoya.
Akaongeza: “Kwa wale wenzangu watoa mimba, nataka wajue ni hatari sana kwani wanaweza kupata matatizo, likiwemo la kutozaa kabisa maishani mwao.”
Aidha, aliongeza kuwa mwanamke anapozaa hupata heshima katika jamii inayomzunguka kwani anaitwa mama, jambo ambalo ni jema.
Irene aliongeza kuwa, kitendo cha kuzaa kinamfanya kuongeza ubize na shughuli za utafutaji wa ‘pesa’ ili kuongeza kipato kwa ajili ya kumlea mwanaye tofauti na mwanamke ambaye hana mtoto.
Akiendelea kutoa ushauri huo, alisema kwamba ikitokea mwanamke akapata ujauzito ambao hakuutarajia asithubutu kuutoa licha ya misukosuko atakayoipata na kuonekana asiyefaa.
“Unajua inapotokea msichana kapata mimba kabla ya kuolewa au akiwa shuleni, ndugu, jamaa na hata jamii itamuona mkosaji lakini hiyo isiwe sababu ya kuitoa kwani mtoto anapozaliwa hupendwa na kila mtu,” alisema Irene.
Kufuatia ushauri huo, Ijumaa liliwaendea hewani baadhi ya mastaa na kuwaambia ushauri huo wa Uwoya na kusikia kutoka kwao ambapo wa kwanza kutoa maoni alikuwa mtangazaji wa runinga Bongo, Maimartha wa Jesse ‘Mai’.
Yeye alisema: “Nikiwa mwanaharakati wa mambo ya wanawake nakubaliana na Uwoya, siwezi kutoa mimba hata siku moja kwani najua madhara yake.”
Mai aliyataja baadhi ya madhara hayo kuwa ni kulegea kizazi au kuharibika kabisa, kuvuja damu kila wakati (internal bleeding), kujiharibia maisha hasa pale unapoingia kwenye ndoa, mwanaume anataka mtoto wewe tayari umeshaharibu kizazi.
Mwanaidi Suka ‘Mainda’;
“Binafsi sijawahi kutoa mimba na sitathubutu kufanya hivyo kwani madhara yake ni kifo, kupoteza fahamu au kutokwa damu nyingi na pia ni kosa la jinai, nawashauri wenye tabia hiyo waache.”
Rehema Fabian, Balozi wa Kiswahili;
“Ukweli nakiri mimi niliwahi kutoa mimba, lakini roho iliniuma sana nikizingatia kwamba, kitendo hicho kinaweza kusababisha kansa ya kizazi au ugumba. Sababu kubwa iliyonisukuma kufanya dhambi hiyo ni kugundua mwanaume mwenyewe hakuwa na msimamo, nikahisi nitailea peke yangu.”
Rose Ndauka;
“Kwa kweli mimi siyo daktari, siwezi kujua madhara ya kutoa mimba, ila kama mtu kanasa bila kutarajia siyo vibaya kuitoa ili asije akazaa mtoto ambaye atakuja kuteseka duniani.”
Naye supastaa mmoja wa filamu Bongo (aliomba jina lake lisitiriwe ili asijenge bifu na Uwoya) alisema kuwa, anamshangaa sana Uwoya kutoa somo hilo wakati na yeye ni staa.
“Heee! Makubwa! Uwoya ndiyo anasema hivyo? Naye si staa? Ina maana anatoa darasa hilo kwa sababu amepata mtoto, nina hakika hata yeye alishawahi kuchoropoa mimba kabla hajaolewa.
“Tusidanganyane, hapa Bongo hakuna staa wa kike ambaye hajawahi kutoa mimba kabla hajaolewa,” alisema staa huyo. |
No comments:
Post a Comment